Miongoni mwa vitu muhimu katika maisha ya mwanadamu ni kupata furaha. Watu wengi wamekuwa na harakati nyingi za kuhakikisha kuwa wanafurahika katika kuishi kwao. Kuna wanaotafuta furaha kupitia kwa rafiki, wapenzi, ndoa zao na hata jamii zao. Ni wazi kwamba kila afanyalo mwanadamu kupitia maamuzi yake, msingi wake huwa ni kutafua furaha, hii haijalishi kama atafanya jambo mbaya au zuri kwa mtazamo wa watu.
Ifahamike, watu wanavuja jasho katika
kufanya kazi kwa sababu wanahitaji mshahara au pato ambalo baadaye hulitumia
katika kufurahi. Wasomi, wafanyabiashara nao wanapohangaka katika hili na lile
ukichunguza utakuta nyuma yao kuna kiu ya furaha.
Hii ina maana kuwa, furaha ndiyo
jambo pekee ambalo watu hulitafuta zaidi. Ni nadra au pengine hakuna mtu ambaye
kwa akili timamu ana kiu ya kupata mabaya na kuhangaika kuyatafuta. Mara nyingi
yakimtokea basi huwa yamejitokeza tu katika safari yake ya kutafuta furaha.
Wezi, majambazi, wazinifu hata watukanaji wote kwa pamoja wanapofanya hivyo
huwa nyuma yao kuna hitaji la kupata furaha.
Pamoja na shabaha ya binadamu kuwa
katika kutafuta furaha, wengi wao wamekuwa hawaipati kwa sababu hawajui njia za
kuipata. Kuna watu wanahangaikia utajiri, wakidhani wakiupata, basi watakuwa na
furaha, lakini baada ya kupata utajiri huo hujikuta hawana furaha. Wengine
huamua kuoa, kuwa na wapenzi na marafiki lakini nao matokeo huwa tofauti na
malengo.
Ingawa kuna matatizo mengi ambayo
yanajitokeza katika maisha ya watu kila siku ambayo huondoa furaha, lakini si
sababu ya moja kwa moja ya kumfanya mtu ahuzunike, eti tu kwa maana kafikwa na
tatizo. Ukichunguza kwa makini utafahamu kuwa furaha si kitu ambacho mtu
anaweza kukipata na kikamtosha. Unaweza kupata kila kitu lakini ukawa huna
furaha.
Ukisema pesa ndiyo furaha, unaweza
kuzipata lakini usifurahike na ukashangaa watu ambao ni masikini wakawa na
furaha tele. Hivyo basi msingi wa furaha ni uelewa wa namna ya kuitafuta na
kuipata. Swali, furaha inapaika wapi na
katika vitu gani? Nibu ni kuishi kwa kuzingatia muongozo ufuatao:
Unaitafutaje furaha?
Watu wengi wanapopata matatizo huwa
hawakubali kuyapokea. Kuna mfano wa mtu mmoja ambaye alikuwa bosi katika
kampuni, siku moja uongozi wa juu uliamua kumshusha cheo kutoka ukurugenzi hadi
mpokea wageni. Bosi huyo alipotelemshwa cheo kwa kiwango hicho hakujiona duni
kwa wafanyakazi wenzake, badala yake alichofikiri yeye ni kwamba watu wote
wanamuunga mkono na kumsikitikia kwa unyama huo wa kushushwa cheo kupitiliza.
Zile fikra za kuhurumiwa na watu
zilimfanya awe na furaha na akawa mtu wa kuwahi kazini kila siku ili watu
wakamuone na kumsikitia, jambo ambalo aliamini kuwa uongozi uliomshusha cheo
ndiyo unaopata aibu mbele ya jamii na wala sio yeye. Kitendo hicho cha kuwahi
kazini na kuonekasna ni mtu mwenye furaha kilimfanya awe mtu wa pekee kwenye
jamii, aliweza kutengeneza maswali mengi kwa watu na hatimaye minong’ono ya kuonewa
ilianza kusikika.
Kilichotokea hatimaye, kampuni moja
kubwa ilipata habari ya kuwepo kwa mtu wa aina hiyo, ikafanya mawasiliano naye
na kumwajiri, bila kujali kashfa zilizokuwa zimemwengua katika wadhifa wake wa
kwanza. Jamaa huyo alipopata ajira mpya alijirekebisha makosa yake ya kugushi
na wizi kwa vile alikuwa amejifunza kilichokuwa kimempata. Bosi huyo aliweza
kuendesha kampuni hiyo kwa mafanikio makubwa, jambo lililowafanya wakuu wake wa
zamani wajute kumuondolea wadhifa.
Hapa tunajifunza kuwa tunapopata
matatizo kinachotufanya tupoteze furaha ni fikra zetu, lakini tukijua kucheza
nazo na kuzielekeza katika mlango wa pili, tunaweza kuyatumia matatizo yetu
kupata furaha pia. Lazima kila mmoja wetu atambue kuwa matatizo ni shule,
tunapoyapata tunajifunza. Lakini hatuwezi kujifunza tukiwa na msongo wa mawazo,
lazima tufanye unafiki fulani wa kimawazo kama alioufanya bosi aliyeshushwa
cheo, yeye hakuangalia wadhifa wake wa zamani, wala namna gani watu wanamtazama
katika kazi yake mpya. Mawazo yanawezaje kutuletea furaha?
Katika hali ya kawaida hakuna mtu
hata mmoja anayeweza kumwambia mwenzake lia naye akafanya hivyo. Kila siku
tunaona na kusikia mengi kutoka kwa
ndugu, rafiki, waalimu wahubiri, wachungaji mapadri wetu na hata kwenye vyombo
ya habari, lakini kusikia huko hakuna maana kuwa ni lazima kutuondolee furaha,
kwani ndani ya akili zetu kuna kitu muhimu ambacho ni maamuzi yetu.
Utawala wa mawazo yetu ni kazi ya
kila siku na uamauzi wa nini ha kufikiri ni suala ambalo lipo kwenye uwezo wa
mwanadamu mwenyewe. Ingekuwa ni lazima kila wazo baya tunaloliona na kulisikia
lazima lituhuzunishe basi tusingekuwa na furaha hata kidogo katika maisha yetu,
kwani hakuna siku ambayo itapita bila kuona, kusikia au kutendewa jambo baya na
mtu mwengine.
Ajali zinatokea kila siku, watu
wanakufa, wanaugua, wanateseka, wanalia, wanaomboleza na kufanyiana hila,
lakini kwa nini hatuyachukulii matukio yote kwa uzito sawa kiasi ha kulia? Ni
kwa sababu tuna uhuru wa kuchagua tulie kwa sababu ya nani na kwa nina? Na hii
ndiyo silaha pekee ya kuyatumia mawazo kutuletea furaha. Yaani kuchagua lipi la
kutuliza na lipi la kutufurahisha na mwisho wa yote tuna uwezo wa kuyatumia
mawazo yetu kuchagua mambo ya kufurahisha na kuyapa kipaumbele, bila kujali ni
mema au mabaya. (Kumbuka mfano wa bosi aliyeshushwa cheo).
Hivyo ni vema wakati tunapokuwa na
mawazo ndani yetu tukazingatia misingi ifuatayo ambayo inaweza kutusaidia kufikia
uamuzi sahihi juu ya kila tunaloona na kulisikia, ili mawazo yasitufanye
tuhuzunike na badala yake tufurahi. Kwanza ni kujipenda wenyewe. Tukijipenda
hatutajihukumu na kujiona duni mbele ya wenzetu na hivyo kutopoteza furaha.
Pili ni kujiamini, kuamini huku kutatuwezesha kuwa na msimamo juu ya maamuzi ya
kila tunachoshibishwa ndani ya mawazo yetu kupitia mawasilia ya sauti na yasiyo
na sauti.
Tatu, kumiliki mawazo yetu
yasichukuliwe na ukubwa au udogo wa tatizo. Udhibiti huu lazima uyaone mambo
yote yanayoingia kichwani kuwa ni ya kawaida kwa vile yapo duniani na
yanawakuta watu kama sehemu ya changamoto za kimaisha. Katika hali ya kawaida
ukubwa au udogo wa tatizo unatokana na mawazo ya mtu husika. Nne, kuwa na
uvumilivu juu ya kila jambo kwa imani kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha.
Tano na mwisho ni kuhakiki maamuzi yetu kama yako sahihi kabla na baada ya
kutenda jambo.