Moja ya nguzo za mafanikio ya wajasiriamali ni
elimu, ikwemo ya kuwaongezea upeo wa kutafuta mitaji.
Ni ijumaa nyingine tunapokutana tena katika
kona hii ya mjasiriamali, hii ni kona ambayo maudhui yake ni kuona namna bora
ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kuanzisha na baadae kuendeleza
biashara zao na kupata mafanikio wanayotamani.
Makala iliyopita ilijadili juu ya umuhimu wa
kuweka akiba ili kujikinga na majanga.
Kuna msemo unasema akiba haiozi, mjasirimali
unapaswa wakati wote kukumbuka msemo huu ili uwe chachu ya wewe kujiwekea akiba
kwa malengo mbalimbali.
Ukiwa na utamaduni wa kujiwekea akiba kutokana
na mapato yako unayoyapata utakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kukabilina na
majanga mbalimbali ambayo yanaweza kutokea katika biashara yako, kumbuka una
nafasi ya kubadilika na kujipanga upya.
Leo katika kona ya mjasiriamali tutakumbushana
juu ya baadhi ya njia ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kuweza
kuongeza mitaji ya biashara zao. Katika njia mbalimbali za kuongeza mitaji zipo
zinazoweza kusaidia na nyingine kuumiza.
Mitaji ya biashara ni kilio cha wengi aidha
kwa wale walio katika ujasiriamali au kwa wale wenye nia ya kuingia kwenye
ujasiriamali. Wengi hulia kwamba watapata wapi mtaji kwaajili ya kuanzisha
biashara au kwaajili ya kuendeleza biashara.
Wajasiriamali wanapaswa waelewe kwamba kuna
njia mbalimbali za kuweza kuongeza mtaji katika biashara wanazofanya. Muhimu
zaidi ni kufahamu njia hizi ili kuweza kuangali ni ipi kwa hatua uliyofikia
inaweza kukusaidia zaidi badala ya kukuumiza.
Yafaa pia kujiuliza je ni sababu zipi
zinazopelekea wewe kuwa na hitaji la ongezeko la mtaji katika biashara
yako na nini matokeo tarajiwa. Kujiuliza
maswali haya na mengine itakusaidi kufanya uamuzi sahii. Zifuatazo ni njia za
kuongeza mitaji ya biashara yako.
Njia ya kwanza ni uwekaji wa akiba. Uwekaji wa
akiba ni njia ya kwanza ambayo inaweza kukusaidia katika kukuza mtaji wako wa
biashara. Kma utakuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ni rahisi kwako kutumia
akiba ili uweze kukuza mtaji wako.
Iwe kwa mjasiriamali mwenye biashara mpya au
inayoendelea ni muhimu sana kufikiria kutumia njia hii ili kuweza kukuza mtaji
wa biashara. Uwekaji wa akiba ni moja ya njia ya kukuza mtaji ambayo haina gharama wala matatizo
kuliko nyingine yoyote.
Uwekaji wa akiba ni njia inayoonekana ngumu
kati ya watu kwasababu ni njia ambayo inahitaji nidhamu ya hali ya juu.
Unapotaka kutumia njia hii ili kuweza kukuza mtaji wa biashara au kuendeleza
biashara unahitaji nidhamu katika matumizi ya fedha zako.
Jiulize je matumizi ya fedha zako yakoje? Ni
yapi yamekuwa matumizi ya msingi na yapi si ya msingi, kwanini usipunguze au
kuacha matumizi yasio ya msingi na kuweka akiba ili kuweza kukuza mtaji
kwaajili ya biashara yako.
Jiulize unatumia kiasi gani cha fedha zako
kwaajili ya ‘vocha’, unatumia kiasi gani kwaajili ya pombe, unatumia kiasi gani
kwaajili ya starehe, vipi michango ya harusi, je unatumia kiasi gani kwaajili
ya burudani nyingine ambazo si za msingi!
Kaa chini na utafakari juu ya mapato na
matumizi yako na angalia ni kwa namna gani unaweza kuweka sehemu ya mapato yako
kama akiba kwaajili ya aidha kukuza mtaji wa biashara unayofanya au kuanzisha
biashara mpya na malengo mengine ya baadae.