Thursday, October 10, 2013

MBINU ZA KUMTEKA MTEJA ASIKUKIMBIE KWENYE BIASHARA YAKO


Namna ya ‘kumteka’ mteja




SIKU zote ni rahisi kumpata mteja ila ni vigumu kumfanya abakie kuwa wako.

Hili ni tatizo kubwa linalowakumba wafanyabiashara wengi, wateja wanakuja kwenye biashara zao mara moja au mbili kisha hawaonekani tena, jambo ambalo limekuwa likiibua hisia tofauti kwa wafanyabiashara.

Wafanyabiashara wengine wanasema wana gundu, wamerogwa au bidhaa ni mbaya. Unakuta mfanyabiashara ana bidhaa nzuri, huduma inaridhisha lakini anashindwa kumfanya mteja anayekuja kwenye biashara yake aendelee kuwa mteja wake wa kudumu.

Hili linatokana na huduma mbaya kwa wateja inayosababishwa na mazingira machafu ya biashara yasiyovutia, vifaa chakavu, lugha mbaya na mteja kutohudumiwa kwa wakati.

Kwa upande mwingine tatizo hili linasababishwa  na   kutokuwa na utashi wa kujua aina za wateja maalumu na namna maalumu ya kuwahudumia kwa maana ya tabia zao na namna ya kuwahudumia.

Wafanyabiashara wengi wamekosa utashi wa kujua aina za wateja, tabia zao na namna ya kuwahudumia, suala linalosababisha kuona kuwa wateja ni watu wa kutanga tanga, hawashikiki au hawana sehemu maalumu ya kununua bidhaa au huduma, jambo ambalo si kweli.

Kutanga tanga kwa wateja kuna sababishwa na wafanyabiashara wenyewe kushindwa kuwafanya waendelee kubaki kuwa wao na wasiende kwingine.

Hapa huna haja ya kwenda kwa mganga ili kumfanya mteja abakie kuwa wako, bali ni kwa kutumia kanuni za kibiashara ambazo ni kuuza bidhaa zenye ubora, kutumia lugha nzuri, kuwa mbunifu, kumpa mteja zaidi ya kile alichokitarajia.

Kwa mfano, wenzetu wanaouza dawa za meno wanaweka zawadi ya mswaki au dawa ndogo ya kuwavutia wateja.

Kwa kina mama wanaotoa huduma ya chakula ukiagiza chakula wanakuletea na matunda kidogo; ndizi au kipande cha parachichi, ambapo haukilipii, ni bure, chakula tu ndicho unalipia.

Kutokana na ubunifu huo wateja wanakuwa wengi kwasababu wanavutiwa na wanahisi kuwa wanapata zaidi ya kile wanachokilipia, wanaridhika na kuifurahia huduma hiyo na wengine wanashindwa kuvumilia kuridhika huko na kufurahishwa, matokeo yake wanawaambia wenzao na wenzao wanawaambia wenzao!

Matokeo yake habari  nzuri zinasambaa kuhusu huduma yako au bidhaa, wateja wanazidi kumiminika, unajikuta umejenga mtandao mkubwa wa wateja na kushinda ushindani ulioko kwenye biashara husika.

Mara nyingi wafanyabiashara wanajisahau katika hili la kumpa mteja zaidi ya kile anachokitarajia, wanafanya hivyo wakati wanaanzisha biashara zao mpya, wakiona biashara imezoeleka kidogo wanasitisha na wateja nao wanakata miguu.

Hapa sizungumzii promosheni bali nazungumzia jambo endelevu litakalomfanya mteja aendelee kuwa wako na asiende kwa mtu mwingine.

Kumpa mteja kitu cha ziada zaidi ya kile alichokuwa anakitarajia kutoka kwako, namaanisha kile kitu ambacho ukimpa hakiwezi kuathiri biashara yako  na hapa ni suala la ubunifu zaidi ndio unahitajika.

Kwa haraka haraka ukiangalia unaweza kuona unapata hasara  lakini  ukifanya uchunguzi wa kina utagundua  kuwa  sehemu hizo zinapata faida kubwa ukilinganisha na idadi kubwa ya wateja wanaokuja katika biashara hiyo na ‘kuwaungisha’.

Sehemu nyingine nimeona wafanyabiashara wanaouza biashara nzuri ila wanakabiliwa na ukosefu wa wateja wa kutosha na kuamua kutumia mbinu ambazo hazizai matunda.

Mfano  unakuta nje ya biashara kuna bango limeandikwa: “Ukimleta mteja akanunua bidhaa tunakulipa.”

Binafsi niliona kuwa mbinu hii haina ushawishi mkubwa na inaonekana kuwa inashurutisha zaidi na ni ya kizamani, wafanyabiashara hao wamekosa utashi wa kibiashara, mbinu za kijasiriamali ambazo wakati mwingine hazihitaji matumizi makubwa ya nguvu ya pesa au mwili, bali ni kufuata mbinu na kanuni za kijasiriamali, kisha utashangaa wateja wanakuja, huna haja ya kutafuta watu wakupigie debe biashara yako.

Mbinu hizo nilizozitaja hapo juu na juhudi  za kuwavutia wateja katika biashara yako zinatakiwa ziambatane na utashi wa kujua aina za wateja, tabia zao  na namna ya kuwahudumia ili uweze kupata mbinu zaidi zitakazokupa nguvu na uwezo wa kumfanya mteja abakie kuwa wako.

Ukizijua aina hizi zitakusaidia kuwavutia wateja na kuliteka soko la biashara kwasababu biashara ni wateja.

Kuna aina sita za wateja maalumu pamoja na tabia zao na jinsi ya kuwahudumia, ambao ni kama wafuatao:

Mteja mkimya ni mteja anayelalamika kimoyo moyo, ukimhudumia mteja huyu vibaya anakuambia hakuna shida lakini ndani ya nafsi yake kuna shida, na hataonekana tena kwenye biashara yako.

Mteja mgomvi ni muwazi na mlalamikaji, unatakiwa umsikilize kwa makini, akikutuma kitu fulani muulize kama atahitaji kingine na kama atakuambia una makosa ukubali.

Wafanyabiashara wengine wanaambiwa kuwa wana makosa wanakataa, wanawaambia wateja: “Nyie hamna hela.”

Wengine huhoji  mbona kulikuwa na hivi miaka mingi lakini sasa havipo, inawezekana ulipata wateja wengi ambao ni wakimya  hawakukuambia ukweli kuhusu huduma za bidhaa yako.

Mteja mgomvi atakusaidia ujue matatizo yaliyoko kwenye biashara yako na kuyatatua.

Mteja mstaarabu hutegemea bidhaa nzuri, hulalamika si kama mkimya, anaweza kukuita na kukueleza, hana maneno mengi, anategemewa asikilizwe, asemi kwa watu wengi  bali anakwenda kuitafuta bidhaa hiyo sehemu nyingine.

Huyu hapendi visingizio, anapenda maelezo yaliyonyooka. Kuna wahudumu au wafanyabiashara wanawaeleza wateja uongo mwingi na hilo tu linatosha kumfukuzisha mteja kwenye biashara yako na unaweza usimuone tena.

Mteja tapeli ni aina nyingine ya mteja ambaye lengo lake ni kujipatia vitu ambavyo hastahili na unaweza kuwajua kwa kuangalia tabia zao, ikiwamo kuuliza bei hata kama anaiona, hupenda kugusa gusa bidhaa, ananung`unika sana, anakuuliza maswali ambayo huwezi kumjibu.

Namna ya kumhudumia ni pamoja na kuzingatia misingi ya taaluma au biashara husika, kutomwacha awe mbali muda mrefu na wewe kwa sababu anaweza kukuta vitu vinavyobebeka akaondoka navyo.

Kitu kingine, usimwonyeshe bidhaa moja kabla hajakupa nyingine, usimwonyeshe bidhaa zaidi ya mbili hiyo inaweza ikawa fursa ya kukuchanganya kwa wingi wa bidhaa ulizompa na kushindwa kujua ni ipi amechukua kwa muda huo anapokurudishia na kukuambia kuwa atakuja siku nyingine au anaweza akawa amenunua ila amezidisha kipimo cha bidhaa zaidi ya pesa aliyoitoa.

Fikiria namna ya kumfanya aendelee kuwa mteja wako, anaweza kuwa mwizi na ni mteja vilevile.

Mteja aliyekubuhu kwa kulalamika ni aina ya mwisho ya mteja anayeweza akawa anakuja njiani huku analalamika kabla hata hajafika dukani, mteja wa aina hii haridhiki kwa lolote hata ukimpa nyongeza anaona ni kidogo.

Usifike mahali ukashindwa kumfanya mteja aendelee kuwa wako kwa sababu ya tabia yake, kwa kuwa tayari una ufahamu na maarifa ya namna ya kumhudumia, hivyo itakusaidia katika kukuza biashara na kufanikiwa zaidi kwa kuwa na wateja wengi ambao hawatakuwa tayari kwenda kwa mfanyabiashara

Source:tanzania daima
Share:

1 comment:

  1. Dawa za asili toka tanga ..zinatibu nguvu za kiume ..UTI sugu..ugumba...vidonda vya tumbo..kurefusha na kunenepesha uume ..miguu kuwaka moto ..uchawi na zindiko..wasiliana na dr kanyat wa tiba asili toka tanga ..0764839091

    ReplyDelete

KUHUSU MMILIKI WA BLOG HII

My photo
Naitwa faraja Mmasa a.k.a Moa,Mkazi na mzaliwa wa Wilaya ya Gairo Morogoro.KARIBU KATIKA BLOG hii tuelimishane mambo mbalimbali.Inatupasa kuwa na ufahamu wa mambo mbalimbali ili tuweze kuyatawala Mazingira yetu .Kuwa na Mwanasheria au Mhasibu haimanishi unatikiwa kujua au kufuatilia maswala ya uhasibu na sheria tu.Mfano nyumba yako au ndoa yako hutaindesha kwa taaluma uliyonayo.Vile vile huwezi kuendesha ujasiliamali kwa mafanikio kwa shahada yako ya uhandisi.TUNAANGAMIA KWA KUKOSA MAARIFA

UJUMBE WA LEO

MIUJIZA MINGI INAYOTOKEA KATIKA MAISHA IPO KATIKA MAWAZO,FIKRA,NA IMANI ALIYONAYO MWANADAMU HUSIKA

USIKOSE KIPINDI HOT JIJINI POWER CLUB ,SIBUKA REDIO 94.5 KILA SIKU SAA SABA MPAKA SAA KUMI

USIKOSE KIPINDI HOT JIJINI POWER CLUB ,SIBUKA REDIO 94.5 KILA SIKU SAA SABA MPAKA SAA KUMI

GAR AD2

GAR AD2

GARI ADVERT

GARI ADVERT

Castrol

Castrol
Powered by Blogger.