Tuesday, August 27, 2013

MIPANGO MIZURI HULETA MAFANIKIO KATIKA UFUGAJI WA NGOMBE WA MAZIWA




Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Wafugaji waliofanikiwa wanafahamu fika kuwa katika uzalishaji wa maziwa 20% inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo.
Watu wengi ambao wanataka kuanzisha ufugaji wa ng’ombe, lakini hawajui ni wapi pa kuanzia. Kwa kawaida, wao wanaweka pesa, kutafuta ng’ombe, kununua na mwisho hupata ng’ombe. Hapo ndipo kuhangaika na kupata msongo wa mawazo kwa mfugaji huanza kwa kuwa ng’ombe hazalishi maziwa kutokana na aina yake pekee.

Kwa wafugaji wadogo walio wengi, wakati ambapo ng’ombe anafika zizini kwake wanakuwa bado hawajawa tayari kumpokea ng’ombe huyo kwa ajili ya ufugaji. Ili ujasiria mali kwa njia ya ng’ombe uweze kufanikiwa na kumfaidisha mfugaji kiuchumi, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa miundo mbinu muhimu inakuwa tayari kabla ya kumleta ng’ombe.


Kwa mujibu wa mwongozi wa kitabu cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Afrika ya mashariki, ng’ombe wa maziwa ni lazima wapate mahitaji yafuatayo:
• Malisho bora na maji safi ya kunywa
• Afya bora bila majeraha
• Mazingira safi ikiwa ni pamoja na  banda lililojengwa vizuri
• Uangalizi mzuri na wa kirafiki,  ambao humfanya ng’ombe kuwa mtulivu bila kuwa na msongo.

Bila mahitaji haya muhimu, na mfugaji kutokumtunza ng’ombe vizuri, asitegemee kuwa ng’ombe huyo atazalisha kiwango kizuri cha maziwa. Uzalishaji wa kiwango cha maziwa na ubora wake unategemeana kwa kiasi kikubwa na mambo hayo yaliyotajwa hapo juu. Wataalamu wanasema kuwa 20% ya uzalishaji wa ng’ombe inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo kutoka kwa mfugaji. Muhudumie ng’ombe wako vizuri naye atarudisha kwa kuzalisha maziwa vizuri.

Mipango

Wafugaji ni lazima wawe na mipango thabiti kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe. Hii hujumuisha idadi ya ng’ombe mfugaji anayotaka kufuga, pamoja na kufahamu ni kiasi gani cha malisho kinachohitajika kwa kipindi chote cha mwaka. Mfugaji pia anapaswa kufahamu kuwa ni kwa namna gani malisho yanafaa kutolewa kwa wanyama.

Mfugaji ni lazima pia apange ni kwa namna gani atapata malisho kwa kipindi chote. Hii inamaanisha kuwa ni muda gani atapanda, kuvuna na kuhifadhi. Mipango ni nguzo muhimu sana kwa kuwa inawezesha kusaidia kufahamu ni nini cha kufanya, namna ya kufikia malengo yaliyokusudiwa, na ni hatua gani imefikiwa. Mfugaji ambaye hana mipango thabiti ni sawa na mtu anayeanza safari bila kufahamu mwisho wa safari yake ni wapi.

Mahitaji ya mlo kamili

Shughuli ya ufugaji wako itakamalika siku ambayo utaweza kuelewa uhusiano kati ya ulishaji wa ng’ombe, uzalishaji wa maziwa na mapato. Endapo ng’ombe wa maziwa atalishwa kwa malisho hafifu ni dhahiri kuwa uzalishaji wa maziwa pia utakuwa hafifu.

Malisho bora

Tafuta ni aina gani ya malisho hufanya vizuri katika ukanda wako. Malisho endelevu hutegemeana kwa kiasi kikubwa na aina ya malisho na utunzaji wake shambani mwako. Chukulia kuwa wewe ni mfugaji mdogo na hauwezi kumudu gharama za umwagiliaji, ni lazima utumie kwa kiasi kikubwa malisho ya wakati wa mvua na kuhifadhi ili kuweza kuyatumia wakati wa kiangazi.

Inashauriwa kupanda majani ya malisho kwa kiasi kikubwa uwezavyo wakati wa mvua. Wahamasishe majirani zako kupanda malisho pia, ili baadaye uweze kununua kutoka kwao. Matete, nyasi, majani ya mtama, majani ya mahindi, lusina, desmodiamu, na alizeti ni miongoni mwa malisho ambayo hufanya vizuri katika maeneo mengi nchini Tanzania.

Kiwango cha kutosha

Fahamu ni kiwango gani kinachotosha kwa kila ng’ombe wako. Hii itakusaidia kufahamu ni kiasi gani cha malisho upande na ni kiasi gani uhifadhi. Kwa wastani, ngombe wa maziwa aliyekomaa mwenye uzito wa kilo 400, anayefugwa ndani ana uwezo wa kula kilo 12 za majani makavu kwa siku. Kumbuka kuwa endapo mifugo yako haitapata malisho ya kutosha wataonesha kwa muonekana wao, na kisha kukupa adhabu kwa kuzalisha maziwa kidogo sana. Kama kanuni inavyoeleza, hakikisha kuwa 15%-18% ya malisho yote ni protini.

Zingatia utunzaji na uzalishaji wa malisho vizuri

Wafugaji walio wengi hukwepa kupanda majani ya malisho kwa kuogopa gharama ya mbolea na mbegu. Kwa uzoefu wetu mfugaji anaweza kutumia mbolea inayotokana na wanyama kupanda malisho na kuyatunza vizuri. Matete ni moja wapo ya malisho hayo. Endapo malisho hayo yatawekwa mbolea vizuri, shamba dogo tu la malisho linaweza kukupatia malisho ya mifugo kwa kipindi chote cha mwaka.

Weka malisho katika hali ya usafi

Hifadhi malisho katika sehemu nzuri, sehemu ambayo hayatapigwa na jua moja kwa moja, mvua au kuwepo uwezekano wa vitu vingine vinavyoweza kuyaharibu kama vile siafu na wadudu wengineo. Majani ya malisho ni lazima yanyaushwe vizuri kuepuka viini vya sumu vinavyoweza kuwepo kwenye malisho. Mfugaji anaweza kuamua juu ya ubora wa malisho kutokana na muonekano wake, harufu na mguso. Malisho mabichi yenye wingi wa majani kuliko shina, yenye kijani kilichokolea, na ambayo yana mguso nyororo, ni moja ya malisho bora ukilinganisha na yale yenye ugumu, shina kubwa na rangi ya njano. Epuka kulisha mifugo yako kwa kutumia malisho yenye ukungu kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.

Kuweka kumbukumbu ni muhimu

Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu lakini huwa hauzingatiwi na wafugaji walio wengi. Baadhi ya wafugaji huona kama uwekaji wa kumbukumbu ni kazi ya ziada, ambayo kulingana na wao haina uhusiano wowote na mapato yanayotokana na shughuli zao. Hata hivyo, bila uwekaji sahihi wa kumbukumbu, mfugaji hawezi kufahamu ni mapato kiasi gani anayopata kutokana na shughuli ya ufugaji. Ni kwa namna gani mfugaji anaweza kufahamu wakati wa kumpandisha ng’ombe wake, kama hajui kuwa zimepita siku ngapi tangu ng’ombe huyo alipozaa!

Source: mkulima mbunifu
Share:

0 comments:

Post a Comment

KUHUSU MMILIKI WA BLOG HII

My photo
Naitwa faraja Mmasa a.k.a Moa,Mkazi na mzaliwa wa Wilaya ya Gairo Morogoro.KARIBU KATIKA BLOG hii tuelimishane mambo mbalimbali.Inatupasa kuwa na ufahamu wa mambo mbalimbali ili tuweze kuyatawala Mazingira yetu .Kuwa na Mwanasheria au Mhasibu haimanishi unatikiwa kujua au kufuatilia maswala ya uhasibu na sheria tu.Mfano nyumba yako au ndoa yako hutaindesha kwa taaluma uliyonayo.Vile vile huwezi kuendesha ujasiliamali kwa mafanikio kwa shahada yako ya uhandisi.TUNAANGAMIA KWA KUKOSA MAARIFA

UJUMBE WA LEO

MIUJIZA MINGI INAYOTOKEA KATIKA MAISHA IPO KATIKA MAWAZO,FIKRA,NA IMANI ALIYONAYO MWANADAMU HUSIKA

USIKOSE KIPINDI HOT JIJINI POWER CLUB ,SIBUKA REDIO 94.5 KILA SIKU SAA SABA MPAKA SAA KUMI

USIKOSE KIPINDI HOT JIJINI POWER CLUB ,SIBUKA REDIO 94.5 KILA SIKU SAA SABA MPAKA SAA KUMI

GAR AD2

GAR AD2

GARI ADVERT

GARI ADVERT

Castrol

Castrol
Powered by Blogger.