Kwa mliotaka
msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa jana tarehe 18 Julai 2013 na Gazeti la
Majira kwamba Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January
Makamba kwamba “Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika
ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia
mtandao huu kutoa majibu ya ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:
Nieleze
kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo itakapofutwa
kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha walau kidogo kwa
maendeleo.
Sitaacha
kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu ambayo wananchi walinichagua kuifanya
ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali ambayo yeye Makamba ni sehemu yake.
Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema ili nchi yetu
iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Ambacho
sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za kusema uongo, kwa
kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea kuhusu suala hili baada
ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili nilianza kulishughulikia bungeni mara
baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi
lukuki za simu ikiwemo hii. Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba
muswada huo wa sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni
‘muswada wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.
Aidha,
sikuishia kusema tu kwa niaba ya wananchi bali nilichukua hatua kwa mujibu wa
kanuni za Bunge nami kuwasilisha jedwali la marekebisho ya kupinga kodi ya
umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine zote zenye kuongeza mzigo wa
gharama za maisha kwa wananchi sio kwenye sekta ya mawasiliano bali pia kwenye
sekta zingine ikiwemo sekta ndogo (sub sector) nyeti ya mafuta.
Mlioniuliza
kwa SMS katika simu na kwenye mitandao ya kijamii sasa ni wakati wa Makamba
kuhojiwa kwa njia hizo hizo kwa kuwa yeye ni sehemu ya Serikali na Serikali
ndiyo ambayo iliingiza suala hili kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge
kupitia hotuba ya Bajeti Serikali na ikalirudia kuliingiza kupitia jedwali la
marekebisho ya Sheria ya Serikali; ni wakina nani hasa kwa majina ndani ya
Serikali na Bunge walioingiza kodi hii? Na ni wakina nani hasa waliopigia kura
ya ndio kuipitisha?
Aidha,
amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo tarehe 19 Julai 2013 akieleza kwamba
hakubaliani na suala hili na kupita kwake ilikuwa na kuzidiwa nguvu. Hivyo,
ataje kwa majina hayo waliozidi nguvu serikali kinyume na matakwa yake.
Amenukuliwa akisema pia kwamba anajua kuwa suala hili haliwezi kutekelezwa na
kwamba ni lazima litabadilishwa kwa kuangalia eneo lingine la kutoza kodi. Ni
vizuri akahojiwa, ikiwa huo ni msimamo wa Serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha
kodi hiyo ni nani na kwanini hajitokezi kutoa agizo la kusitisha wakati
maandalizi yakiendelea ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa kodi hiyo
katika mkutano ujao?
Wakati Naibu
Waziri akisema hayo, Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa katika Serikali hiyo
hiyo yeye ametoa kauli tofauti siku hii hii ya leo ambapo kwa mujibu wa gazeti
la Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao ya simu nchini na watanzania kwa
ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya sh 1000 kwa mwezi kwa kila laini ya simu
za kiganjani.
Na kwa kuwa
amesema kwamba Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau, natoa mwito
kwa wananchi kumtumia maoni kupitia namba zake za simu za mkononi
0754/0684-765644.
Aidha, ni
vizuri aeleze subira hiyo ivutwe mpaka lini? Na ni wakina nani hasa kwa majina
waliomfanya akaingiza kodi hiyo katika kitabu cha Hotuba yake aliyosoma bungeni
kuhusu bajeti ya Serikali na wakina na hasa kwa majina waliomfanya arejeshe
kodi hiyo ya kadi za simu kwenye jedwali la marekebisho ya muswada wa sheria ya
fedha alilowasilisha bungeni.
Nasisiza
kuwa kauli za ujumla za Serikali bila kuwataja kwa majina wahusika ni za
kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na
nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge. Ni muhimu badala ya kutoa kauli
za ujumla za kulaumu wabunge, Rais ama kiongozi mwingine mwenye mamlaka
ajitokeze kusitisha kutozwa kwa kodi hiyo na kuanzisha mchakato wa muswada wa
kufuta kodi hiyo kuwasilishwa katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza
tarehe 27 Agosti 2013.
Majina ya
wahusika yasipotajwa au mamlaka zinazohusika zisipotoa kauli katika mkutano wa
hadhara nitakaoshiriki jumapili tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara
kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni nitatoa mrejesho kuhusu
yaliyojiri katika mkutano uliopita wa Bunge na kueleza hatua zaidi zinazopaswa
kuchukuliwa kuwezesha majina ya wabunge hao kutajwa hadharani na hatua za
kuondoa kodi hiyo kuchukuliwa.
Uongozi bora
na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya ukuaji endelevu wa
uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi. Twende kazi.
John Mnyika
(Mb)
0 comments:
Post a Comment