Mipango
thabiti huleta mafanikio katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Wafugaji
waliofanikiwa wanafahamu fika kuwa katika uzalishaji wa maziwa 20% inatokana na
aina ya ng’ombe na 80% matunzo.
Watu wengi
ambao wanataka kuanzisha ufugaji wa ng’ombe, lakini hawajui ni wapi pa kuanzia.
Kwa kawaida, wao wanaweka pesa, kutafuta ng’ombe, kununua na mwisho hupata
ng’ombe. Hapo ndipo kuhangaika na kupata msongo wa mawazo kwa mfugaji huanza
kwa kuwa ng’ombe hazalishi maziwa kutokana na aina yake pekee.
Kwa wafugaji
wadogo walio wengi, wakati ambapo ng’ombe anafika zizini kwake wanakuwa bado
hawajawa tayari kumpokea ng’ombe huyo kwa ajili ya ufugaji. Ili ujasiria mali
kwa njia ya ng’ombe uweze kufanikiwa na kumfaidisha mfugaji kiuchumi, mfugaji
ni lazima ahakikishe kuwa miundo mbinu muhimu inakuwa tayari kabla ya kumleta
ng’ombe.
Kwa mujibu
wa mwongozi wa kitabu cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Afrika ya mashariki,
ng’ombe wa maziwa ni lazima wapate mahitaji yafuatayo:
• Malisho
bora na maji safi ya kunywa
• Afya bora
bila majeraha
• Mazingira
safi ikiwa ni pamoja na banda
lililojengwa vizuri
• Uangalizi
mzuri na wa kirafiki, ambao humfanya
ng’ombe kuwa mtulivu bila kuwa na msongo.
Bila
mahitaji haya muhimu, na mfugaji kutokumtunza ng’ombe vizuri, asitegemee kuwa
ng’ombe huyo atazalisha kiwango kizuri cha maziwa. Uzalishaji wa kiwango cha
maziwa na ubora wake unategemeana kwa kiasi kikubwa na mambo hayo yaliyotajwa
hapo juu. Wataalamu wanasema kuwa 20% ya uzalishaji wa ng’ombe inatokana na
aina ya ng’ombe na 80% matunzo kutoka kwa mfugaji. Muhudumie ng’ombe wako
vizuri naye atarudisha kwa kuzalisha maziwa vizuri.
Mipango
Wafugaji ni
lazima wawe na mipango thabiti kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe. Hii hujumuisha
idadi ya ng’ombe mfugaji anayotaka kufuga, pamoja na kufahamu ni kiasi gani cha
malisho kinachohitajika kwa kipindi chote cha mwaka. Mfugaji pia anapaswa
kufahamu kuwa ni kwa namna gani malisho yanafaa kutolewa kwa wanyama.
Mfugaji ni
lazima pia apange ni kwa namna gani atapata malisho kwa kipindi chote. Hii
inamaanisha kuwa ni muda gani atapanda, kuvuna na kuhifadhi. Mipango ni nguzo
muhimu sana kwa kuwa inawezesha kusaidia kufahamu ni nini cha kufanya, namna ya
kufikia malengo yaliyokusudiwa, na ni hatua gani imefikiwa. Mfugaji ambaye hana
mipango thabiti ni sawa na mtu anayeanza safari bila kufahamu mwisho wa safari
yake ni wapi.
Mahitaji ya
mlo kamili
Shughuli ya
ufugaji wako itakamalika siku ambayo utaweza kuelewa uhusiano kati ya ulishaji
wa ng’ombe, uzalishaji wa maziwa na mapato. Endapo ng’ombe wa maziwa atalishwa
kwa malisho hafifu ni dhahiri kuwa uzalishaji wa maziwa pia utakuwa hafifu.
Malisho bora
Tafuta ni
aina gani ya malisho hufanya vizuri katika ukanda wako. Malisho endelevu
hutegemeana kwa kiasi kikubwa na aina ya malisho na utunzaji wake shambani
mwako. Chukulia kuwa wewe ni mfugaji mdogo na hauwezi kumudu gharama za
umwagiliaji, ni lazima utumie kwa kiasi kikubwa malisho ya wakati wa mvua na
kuhifadhi ili kuweza kuyatumia wakati wa kiangazi.
Inashauriwa
kupanda majani ya malisho kwa kiasi kikubwa uwezavyo wakati wa mvua.
Wahamasishe majirani zako kupanda malisho pia, ili baadaye uweze kununua kutoka
kwao. Matete, nyasi, majani ya mtama, majani ya mahindi, lusina, desmodiamu, na
alizeti ni miongoni mwa malisho ambayo hufanya vizuri katika maeneo mengi
nchini Tanzania.
Kiwango cha
kutosha
Fahamu ni
kiwango gani kinachotosha kwa kila ng’ombe wako. Hii itakusaidia kufahamu ni
kiasi gani cha malisho upande na ni kiasi gani uhifadhi. Kwa wastani, ngombe wa
maziwa aliyekomaa mwenye uzito wa kilo 400, anayefugwa ndani ana uwezo wa kula
kilo 12 za majani makavu kwa siku. Kumbuka kuwa endapo mifugo yako haitapata
malisho ya kutosha wataonesha kwa muonekana wao, na kisha kukupa adhabu kwa
kuzalisha maziwa kidogo sana. Kama kanuni inavyoeleza, hakikisha kuwa 15%-18%
ya malisho yote ni protini.
Zingatia
utunzaji na uzalishaji wa malisho vizuri
Wafugaji
walio wengi hukwepa kupanda majani ya malisho kwa kuogopa gharama ya mbolea na
mbegu. Kwa uzoefu wetu mfugaji anaweza kutumia mbolea inayotokana na wanyama
kupanda malisho na kuyatunza vizuri. Matete ni moja wapo ya malisho hayo.
Endapo malisho hayo yatawekwa mbolea vizuri, shamba dogo tu la malisho linaweza
kukupatia malisho ya mifugo kwa kipindi chote cha mwaka.
Weka malisho
katika hali ya usafi
Hifadhi
malisho katika sehemu nzuri, sehemu ambayo hayatapigwa na jua moja kwa moja,
mvua au kuwepo uwezekano wa vitu vingine vinavyoweza kuyaharibu kama vile siafu
na wadudu wengineo. Majani ya malisho ni lazima yanyaushwe vizuri kuepuka viini
vya sumu vinavyoweza kuwepo kwenye malisho. Mfugaji anaweza kuamua juu ya ubora
wa malisho kutokana na muonekano wake, harufu na mguso. Malisho mabichi yenye
wingi wa majani kuliko shina, yenye kijani kilichokolea, na ambayo yana mguso
nyororo, ni moja ya malisho bora ukilinganisha na yale yenye ugumu, shina kubwa
na rangi ya njano. Epuka kulisha mifugo yako kwa kutumia malisho yenye ukungu
kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.
Kuweka
kumbukumbu ni muhimu
Uwekaji wa
kumbukumbu ni muhimu lakini huwa hauzingatiwi na wafugaji walio wengi. Baadhi
ya wafugaji huona kama uwekaji wa kumbukumbu ni kazi ya ziada, ambayo kulingana
na wao haina uhusiano wowote na mapato yanayotokana na shughuli zao. Hata
hivyo, bila uwekaji sahihi wa kumbukumbu, mfugaji hawezi kufahamu ni mapato
kiasi gani anayopata kutokana na shughuli ya ufugaji. Ni kwa namna gani mfugaji
anaweza kufahamu wakati wa kumpandisha ng’ombe wake, kama hajui kuwa zimepita
siku ngapi tangu ng’ombe huyo alipozaa!
Source: mkulima mbunifu
0 comments:
Post a Comment