Unaweza
kutunza kuku wa kienyeji na ukawa na kipato cha uhakika, pamoja na lishe nzuri
kwa ajili ya familia.
Ulishaji: Kuku wa kienyeji wanaweza kulishwa
kwa kumia mahindi, mchele, na mabaki ya ugali. Vyakula hivi ni lazima vikaushwe
vizuri na kusagwa vizuri. Ulishaji ni lazima ufanyike katika sehemu safi au kwa
kutumia vyombo vilivyotengenezwa maalumu kwa ajilii ya kulishia kuku.
Banda: Kuku
wawe wa kienyeji au wa kisasa, wanahitaji kuwa na banda zuri kwa ajili ya
malazi na kuwalinda. Wanahitaji chumba chenye nafasi ya kutosha na
kinachopitisha hewa ya kutosha. Ni lazima kuwawekea fito kwa kuwa ndege hupenda
kupumzika juu ya fito. Ni lazima banda la kuku lifungwe vizuri nyakati za usiku
ili kuzuia wanyama wanaoweza kuwadhuru kuku. Ni lazima liwe safi wakati wote
ili kuzuia magonjwa kama vile mdondo na mengineyo. Usitumie pumba za mbao au
nguo kuukuu kwenye viota vya kutagia kwani huchochea kuwepo utitiri na funza wa
kuku. Inashauriwa kutumia mchanga laini.
Maji ya
kunywa: Kuku wapatiwe maji safi. Ni lazima kuangalia mara kwa mara na
kuyabadilisha maji. Kamwe usiwape kuku maji machafu.
Chanjo:
Chanjo kwa mifugo ni lazima ili kuzuia mashambulizi ya magonjwa. Magonjwa
yaliyozoeleka ni kama vile Mdondo, Kideri, Ndui ya kuku, na homa ya matumbo
(typhoid). Chanjo kwa kawaida hutolewa mara moja kwa kila baada ya miezi
miwili.
Uwekaji wa
kumbukumbu: Kumbukumbu zijumuishe aina ya ulishaji, namba ya uzalishaji, muda
wa mwisho wa matumizi, kiasi cha malisho kwa kila siku, idadi ya vifo, na idadi
ya mayai yaliyozalishwa.
Mwanzoni
unahitaji nini?
Wafugaji
walio wengi wanauliza wanahitaji nini katika hatua za awali ili kuweza
kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku. Hii itategemea aina ya kuku uliochagua
kufuga.
Ni busara
kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika na viwe katika hali ya usafi kabla ya
kuweka kuku bandani mwako. Kama unaanza na vifaranga, vifuatavyo ni vifaa
muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya vifaranga 200.
• Tenga na
utengeneze banda zuri lenye joto na hewa ya kutosha wakati wote.
• Vyombo
vinne (4) vya kunyweshea maji, hii ni katika wiki 2 za mwanzo na uongeze vyombo
taratibu kulingana na kuku wanavyokua.
• Vyombo
vinne (4) vya kulishia chakula, na viongezeke kulingana na kuku wanavyokua.
• Matandazo
makavu na safi, inaweza kuwa maranda au mabua ya ngano.
• Pakiti
moja au mbili za dawa ya Coccid (hii inapatikana katika maduka yote ya kilimo).
Hata hivyo, utaratibu wa chanjo ni lazima ukamilishwe.
• Chakula
kwa ajili ya vifaranga ambacho kimezalishwa na watengenezaji wanaoaminika.
Ufugaji wa
kuku unaweza kuongeza kipato cha familia
“Mimi ni mfugaji mdogo wa kuku wa kienyeji
katika viunga vya jiji la Dar es Salaam. Nina kuku 65 ambao ninawafuga katika
eneo dogo nyumbani. Nilivutiwa kuanza ufugaji wa kuku wa kienyeji baada ya
kutumia fedha nyingi kununua mayai ya kuku wa kienyeji kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani.
Nilikua
natumia zaidi ya shilingi elfu thelathini (30000) kila mwezi kwa ajili ya
kununua mayai ya kuku. Ndivyo anavyoanza kusimulia mafanikio yake Bi. Haika
Mcharo, ambae ni mfugaji.
Msukumo huu
ndio ulinifanya niwe na wazo la kufuga kuku wa kienyeji. Nilianza na kuku 12 na
sasa ninao kuku 65 wanaotaga na wanaotarajia kutaga. Sipati faida kubwa sana
ila kwa sasa sinunui tena mayai bali ninauza mayai. Faida nyingine ni upatikanaji
wa mbolea unaotokana na kinyesi cha kuku. Ninatumia kwa kulimia bustani ya maua
na mboga mboga, pia majirani wenye uhitaji wanakuja kwangu kubeba. Kwangu,
kufuga kuku wa kienyeji kuna umuhimu sana kwani najiongezea kipato, ni kama
akiba ambapo faida yake huzaana tu kama riba ya benki.
Malengo yangu ni kuwa na kuku wengi ambao
watagharamia karo ya watoto wangu, malipo ya hospitali na gharama nyingine za
nyumbani. Sihangaiki sana katika kupata chakula cha kuku ninaowafuga kwani
mbali na mchanganyiko wa chakula ninaowanunulia kwa jina maarufu layers mash
pia huwapa mabaki ya chakula, majani, mabaki kutoka jikoni na, vyakula vya
kujitafutia muda wa jioni napowafungulia. Mfumo huu wa kufuga kuku kwa njia ya
kienyeji unatumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi. Huwa ninazingatia tiba
mara ninapoona kuku wangu wanadhoofika. Nina daktari maalumu wa mifugo ambaye
hunipa ushauri wa tiba ipi niitumie na kwa wakati gani. Pia ninazingatia chanjo
zote ili kuwalinda na magonjwa.
Hakuna
changamoto kubwa ninayokumbana nayo bali hali ya kuwatunza na kuwalisha
inahitaji umakini mkubwa ili wakue na kupata kile ninachokitarajia. Ufugaji wa
kuku wa kienyeji ni rahisi na hauhitaji gharama kubwa kwani waweza ukafuga kama
kikundi au mtu mmoja mmoja. Nimefanikiwa kuwashawishi akina mama 5 ambao kwa
sasa wameanza ufugaji wa kuku wa kienyeji. Lengo ni kuwa na kikundi ambacho
tunaweza kupata soko la kuuza mayai kwa uhakika na upatikanaji wake uwe wa
uhakika
source;mkulima mbunifu
Hili somo ni nzuri sana lakini nahitaji kuona mchanganuo mzima wa gharama za ufugaji kuku.
ReplyDelete