Katika
safari ya maisha, ni jambo la kawaida kabisa kukutana na vikwazo vinavyoweza
kukatisha tamaa. Ukubwa wa vikwazo au changamoto hizo, zinaweza kukusababishia
ukaiona dunia kama imegeuka, au wakati mwingine ukatamani ipasuke uingie ndani
yake.
Yapo mambo
mengi yanayoweza kukufanya ufikirie hivyo. Huenda yakawa ni makosa ya
kibinadamu, matatizo, changamoto, kukatishwa tamaa na baadhi ya watu au
kujiponza mwenyewe kutokana na hili au lile. Lakini ukikaa chini, ukatafakari
utatambua kuwa hakuna binadamu asiyeteleza kwa kufanya makosa au kupitia
changamoto kwenye safari ya maisha.
Hivyo wakati
mwingine unapaswa kuelewa kuwa kwa kila linalokupata, bado unayo nafasi ya
kufungua ukurasa mpya. Kupatwa na mitihani katika maisha, mara nyingi ni darasa
mojawapo tunalotakiwa kuliangalia kwa umakini ili kupata somo au fundisho
lililo ndani yake.
Ikiwa
mtihani huo umekuja kutokana na kosa ulilofanya, ni vyema kukubali kama
umekosea na kisha kujipa nafasi ya kusonga mbele. Tunaelewa kuwa maisha ya kila
mmoja wetu kwa namna moja au nyingine yanaendeshwa na misimamo mbalimbali. Kuna
wale wanaoamini kuwa wao hawawezi kufanya
jambo Fulani na wakati mwingine kuamini kuwa hawawezi kukosea kabisa.
Ni sawa
lakini tukumbuke kwamba hakuna binadamu aliyekamilika kwa kila mmoja wetu
anaweza kuteleza na kufanya kosa bila kukusudia . Hivyo basi kwa namna yoyote
ile katika maisha yetu kutenda makosa ni sehemu ya maisha. Ni vyema kujifunza
kukubali kama umekosea na kujirekebisha.
Pili, jifunze kutokana na lile kosa. Si dhani
kama leo ukikosea jambo Fulani unaweza kulirudia kosa kama lile siku nyingine.
Hata kama ikitokea labda kwa namna nyingine tena. Nakumbuka wakati nikiwa mdogo
baba yangu aliniletea zawadi kama pongezi ya kufanya vizuri darasani.
Siku hiyo aliponiletea tulikuwa tumekaa na
kaka zangu. Alinikaribisha tukiwa pamoja ili iwe chachu kwa wao kufanya vizuri
pia. Au pengine kuwafanya waone wivu na wao waweze kufanya vizuri wakiwa
shuleni. Basi alinipa ile zawadi. Wakati wa kupokea nilifanya kosa kwa kupokea
na mkono wa kushoto. Kwa ukali aliniambia nirudishe ile zawadi akaondoka nayo.
Baada ya
kutafakari kwa muda nikakumbuka kumbuka kuwa nilifanya kosa kupokea na mkono wa
kushoto kitendo ambacho alishawahi kutusisitizia kuwa siyo cha heshima. Lile
lilikuwa funzo kwangu kwani mpaka leo sikuwahi kufahamu ile zawadi ilikuwa ni
ya aina gani, kwani ilikuwa imefungwa.
Baada ya
kutokea kwa kadhia ile na kuweza kugundua kosa langu, moja kwa moja nilienda
kuomba msamaha kwa baba. Tangu siku ile sikuwahi tena kumpa au kupokea kitu
chochote na mkono wa kushoto. Hata ikitokea hivyo kama nimejisahau lazima
nitaomba radhi.
Ninachoamini
mimi ni kwamba kwa hali yoyote ile ni lazima tuyape nafasi maisha yaendelee.
Hivyo hatuna haja ya kuangalia nyuma pale tunapojikwaa, kwani utakachoambulia
hapo ni maumivu tena inawezekana ukaumia hapo kuliko awali.
Wapo
waliofikia kufanya maamuzi ya ajabu baada ya kukutwa na mtihani au kufanya
makosa katika jamii. Wengine hata waliweza kutengwa kutokana na makosa yao.
Lakini kushindwa kwao kukubali makosa waliyotenda, kulizaa matatizo mengine.
Kwani utakuta ili kuondoa aibu iliyo mbele yao, waliamua kukimbia miji yao na
hivyo kwenda kuanza maisha sehemu nyingine.
Suluhisho
pekee la jambo kama hili ni kuomba msamaha na kujipanga upya. Usikubali kukata
tamaa kwa kuanguka mara moja, hata ukianguka mara tatu bado unayo nafasi ya
kusimama na kuanza upya na kufanya vizuri hata pengine kuliko mwanzo. Kitu
kikubwa jiamini kisha chukua jukumu la kusonga mbele kwa kujiamini zaidi,
utabadili maisha yako na utafanikiwa.
Makala hii
imeandikwa na Suzan Mwillo wa Gazeti la Mwananchi.
Mawasiliano
suzanmwillo@gmail.com
0 comments:
Post a Comment