VITUKO na matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA
vimeendelea kushika kasi.
Jana Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa
na bomu la machozi lililorushwa na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika
mkutano ulioitishwa na chama hicho.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye
viwanja vya Sahara ambapo bomu hilo lilimpata mtu aliyekuwa karibu na
Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja.
Baada ya kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka
kumchukua majeruhi huyo ili wamweke kwenye gari lao apelekwe hospitalini,
lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo
kilichofanywa na askari hao kililenga kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na
matakwa ya wafuasi wa CHADEMA waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali
ambako hali yake inadaiwa inaendelea vizuri.
Akielezea hali ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine
uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi walifika katika viwanja vya
Sahara wakiwa na magari matatu kwa lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA
wasifanye mkutano wakidai haukuwa na baraka za jeshi hilo.
Mnyika alisema polisi hao walisema sababu ya kuuzuia
mkutano huo ni uwepo wa ziara ya Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni,
hivyo walikuwa wameelekeza nguvu zao katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na
uwezo wa kuulinda mkutano wa CHADEMA.
“Nikiwa nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi
walikuja kusema tuache tusifanye mkutano, nilisogea karibu na gari
kumlalamikia ofisa wa polisi kwani kitendo cha kuahirisha mkutano kwa barua
waliyoileta saa sita mchana siku ya mkutano wakati sisi tuliwapa taarifa
siku nne zilizopita ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa
najadiliana kwa simu na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam na Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema kumlaumu kutumika
vibaya kwa Jeshi la Polisi.
“Nilipokuwa bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu
lilirushwa kutoka ndani ya gari ya polisi na kupita karibu na mimi
likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu, ki ukweli nimeshangazwa sana na
matumizi mabaya ya silaha za moto,” alisema.
Aliongeza kuwa katika purukushani zilizotokea baada ya
bomu kupigwa, alipoteza nyaraka mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi
kuwaonyesha wafuasi wa chama hicho hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge
wake walivyopitisha kodi ya huduma za simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa anena
Aidha katika mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa
ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza
kuhutubiwa naye kwa kile alichosema kuwa watu wake wa usalama walimwambia
mapema hali si salama kwenye mkutano huo.
“Nilipata taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi
walikuwa na mpango wa kuleta fujo, hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda
nisingeenda kuhutubia, pengine bomu lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu
au kwa mwingine,” alisema Dk. Slaa alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya
simu baada ya kutoonekana mkutanoni.
Zuio la polisi
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana
liliahirisha mkutano huo wa CHADEMA kabla viongozi hao kupanda jukwaani.
Liliwapelekea barua ya zuio CHADEMA inayosomeka:
“Kumbuka barua ya tarehe 17 Julai, yenye kumb. CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013
uliyomwandikia Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam. Kamishna wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam amezuia kufanyika kwa mkutano huo
tarehe 21 Julai 2013 katika viwanja vya Sahara, Mabibo kwa sababu siku
mliyoomba kufanya mkutano wenu wa hadhara, Wilaya ya Kinondoni ina mapokezi
ya ugeni wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Hata hivyo Mnyika alipinga sababu hiyo ya polisi kwa
madai CHADEMA wamepeleka taarifa kwa Jeshi la Polisi tangu Julai 17 kwamba wangefanya
mkutano katika viwanja hivyo Julai 21, lakini jeshi hilo halikuwajibu hadi
walipokuwa wanaenda mkutanoni.
CHADEMA wabadili mbinu
Kutokana na kuzuiwa kufanya mkutano kwenye viwanja vya
Sahara, CHADEMA waliamua kuufanyia Ubungo kutokana na kuomba vibali viwili
kwenye maeneo tofauti.
Baada ya kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo kilikuwa
halali, hivyo Mbunge wa Ubungo aliyekuwa amefika Sahara kwa ajili ya
kuhutubia, aliandamana kwa miguu na wafuasi wa chama hicho hadi Ubungo,
huku kukiwa na makachero wengi wa polisi waliofuatilia maandamano hayo.
Akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika
Ubungo, Mnyika alisema polisi walifanya kitendo cha kikatili, kusubiri watu
wamalize maandalizi, wakusanyike uwanjani ndipo wanaleta barua ya kupiga
marufuku mkutano kwa kisingizio kuwa katika Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na
ziara ya makamu wa Rais katika Jimbo la Kawe na Kindondoni.
“Sisi tupo Ubungo, Makamu wa Rais yupo Kawe na
Kinondoni, sasa suala la kuzuia mikutano isifanyike lilikuwa na maana gani?
Kama Jeshi la Polisi walisema hawana askari wa kutosha kulinda mkutano wetu
mbona katika kuutawanya wamekuja na magari matatu?” alihoji.
Mnyika alitumia muda mwingi kulilaumu Jeshi la Polisi,
kwanza kwa kuahirisha mkutano muda mfupi kabla ya viongozi kupanda jukwaani,
lakini pia kitendo cha kurushwa bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote.
Madudu zaidi ya CCM
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameendelea kuanika
madudu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), safari hii akitoa nyaraka za mikakati
ya chama hicho tawala kufundisha vijana kukabiliana na wapinzani.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi katika Viwanja vya
Mahakama ya Mwanzo, Nguzo Nane, mjini Shinyanga, Mbowe alisema kuwa ili
kujilinda dhidi ya vitendo alivyodai wanafanyiwa na vijana wa Green Guards
- kikosi cha vijana wa CCM, chama chao kitaendelea na mipango ya kuwapatia
vijana wao mafunzo ya ukakamavu.
Mbowe alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa
chama hicho tawala kupitia wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) kimekuwa
kikitoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha
kuwa moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kukabiliana na upinzani.
“Tunashambuliwa, watu wetu wanapigwa, wanateswa,
wanatekwa na wengine kuuawa, kwa sababu tu wanataka mabadiliko na wanapenda
CHADEMA, majuzi mlisikia Waziri Mkuu Pinda anasema wamechoka...sasa
tunasema Pinda kama umechoka ondoka upishe ofisi ya umma hiyo, upishe
kwenye ofisi ya watu kama umechoka, maana kuchoka huko ni kuchoka kwa CCM.
Pisheni ofisi sio za kwenu hizo, ni za Watanzania.
“Wananchi hapa mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM,
moja ni cheti cha kuhitimu mafunzo na nyingine hapa juu imeandikwa ‘Sera za
Msingi za CCM’, sasa mi sitawasomea, naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote
anayejua kusoma, awasomee mjue tunaposema CCM wamekuwa na kikundi
kinachoshambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua Watanzania wenzao eti
tu kwa sababu wanaunga mkono CHADEMA, huwa tunamaanisha nini,” alisema
Mbowe.
Mmoja wa wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara,
ambao ulikuwa ni sehemu ya shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya
Ziwa Mashariki (mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa
na kusoma sehemu inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho.
Gazeti hili pia lilifanikiwa kuona kabrasha hilo kwa
karibu, ambapo kifungu cha 9.1 kinachozungumzia UVCCM, kinasomeka hivi;
“(i) Umoja wa vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana
katika itikadi, ukakamavu na mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana
wenye ari ya kutimiza wajibu wao wakiwa walinzi wa chama, viongozi na
wagombea wa CCM.
“(i) Utaratibu wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe
kwa dhati. Chama kiwe na mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi
watakaofaa kuwapatia vijana mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya
uchaguzi/uraia. Mafunzo ya makambi ya vijana, mbali ya kujifunza nyimbo za
hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na
vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani.”
Mbowe pia aliwaonyesha wananchi waliofurika kwenye
mkutano huo cheti cha mmoja wa watu waliohitimu mafunzo ya makambi ya
vijana wa CCM ambacho kilionyesha mhusika alianza mafunzo Juni 27, 2009 na
kumaliza Julai 4, 2009, mkoani Dodoma.
Cheti hicho kimesainiwa na watu wawili, mmoja mwenye
jina la Jumanne Kitundu, akiwa na nafasi ya Katibu wa UVCCM, Dodoma mjini
na mwingine, Robert Mwinje, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Wilaya ya Dodoma
mjini.
Cheti hicho kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa)
alihitimu mafunzo ya masomo ya kanuni ya umoja wa vijana, wajibu wa vijana
katika chama, ulinzi na usalama, ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana
katika uchaguzi, rushwa, ukimwi, historia ya TANU na ASP pamoja na maadili.
Msimamo wa CHADEMA
Mbowe alisitiza kuwa CHADEMA kitasimamia azimio la kikao
cha Kamati Kuu ya chama hicho juu ya kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na
usalama ikiwemo kuanzisha makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wa
chama hicho watakaokuwa na jukumu la kulinda viongozi wao.
Ingawa msimamo huo umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali
likiwemo Jeshi la Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na CCM, Mbowe
amesisitiza kuwa hawatarudi nyuma juu ya mpango huo utakaoimarisha ulinzi.
Kodi ya laini za simu
Hoja ya tozo ya simu imekuwa ajenda kubwa kwenye
mikutano iliyofanywa na viongozi mbalimbali wa CHADEMA.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA),
John Heche alisema kama wananchi wasingeipa ushirikiano CHADEMA na kupinga
maovu mbalimbali, CCM ingekuwa imeshauza nchi na wananchi wake.
Alisema tozo la laini za simu lilipitishwa wakati
wabunge wa CHADEMA walipokwenda Arusha kushiriki maombolezo na mazishi ya
marehemu wa tukio la bomu, hivyo serikali ikaona ipeleke jambo hilo
lililobarikiwa na wabunge wengi wa CCM.
“Maana yake ni nini? Kodi hii kwanza mwananchi maskini
kabisa ambaye amedunduliza na kununua simu, atakuwa analipa sawa sawa na
matajiri wakubwa, yaani wewe hapa utakuwa unalipa kodi sawa na Reginald
Mengi...lakini kama hiyo haitoshi, ukipiga mahesabu utakuwa unalipa kodi
takriban shilingi 12,000 kwa mwaka.
“Serikali hii ya CCM inayowaletea kodi ya sh 12,000 kwa
mwaka ndiyo ililazimika kuondoa na kufuta kodi ya kichwa, baada ya CHADEMA
kuwa imefanya hivyo kwenye halmashauri zake, kwa kuanza na Hai ambako
Mwenyekiti Mbowe alikuwa ni mbunge na Karatu kwa Dk. Slaa. Sasa walifuta
kodi ya manyanyaso ya kichwa kwa maelekezo ya CHADEMA iliyokuwa sh 3,000
kwa mwaka, ambapo watu walikuwa wanakimbia nyumba na kujificha maporini,
wengine wakaliwa na wanyama, sasa wanataka mlipe kimya kimya, sh 12,000 kwa
mwaka. Ni matokeo ya kushindwa kwa sera za CCM,” alisema Heche.
Mkutano wa Geita
Wabunge wa CHADEMA wanaotoka Kanda ya Ziwa na viongozi
wa chama hicho nao waliendelea kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali
huku wakilalamikia tozo la laini za simu pamoja na mapendezo ya rasimu ya
katiba mpya yaliyotolewa na CCM hivi karibuni yakipinga mambo mengi
yaliyopendezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jana, wabunge hao wa viongozi walifanya mikutano ya
hadhara katika mji wa Kasamwa huko Geita na Sengerema mkoani Mwanza ambako
walisema CCM imekosa sifa ya kuongoza ndiyo maana maisha ya Watanzania yamezidi
kuwa magumu kadiri siku zinavyokwenda mbele.
Wabunge hao pamoja na viongozi na makada wa CHADEMA
ambao wapo kwenye msafara wa kuimarisha chama katika kanda hiyo, ni pamoja
na Ezekiel Wenje (Mbunge wa Nyamagana), Profesa Kulikoyela Kahigi
(Bukombe), Dk. Anthony Mbasa (Biharamulo Magharibi) na Conchesta Rwamlaza
(Viti Maalumu – Kagera).
Viongozi na makada wengine ni pamoja na mjumbe wa Baraza
Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar Kashaga, katibu wa CHADEMA Manispaa ya
Bukoba, Lenatus Kilongozi pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya ya Biharamulo
Magharibi, George Kasaiza.
Akizungumza kwenye mikutano hiyo, Wenje alisema CHADEMA
inatarajia kuunda mabaraza ya wananchi kuhusu muundo wa serikali tatu, na
wanatarajia kukusanya saini za Watanzania kupinga tozo ya kodi mpya ya
laini za simu iliyopitishwa hivi karibuni bungeni.
Alisema kwa sasa CCM wametoa mapendekezo ya kutaka
kusiwepo uwazi wa mikataba, maadili ya umma na haki za binadamu kwenye
katiba mpya, na inataka Spika wa Bunge lazima atokane na mbunge, jambo
aliloliita ni kuendeleza ukandamizaji kwa wananchi.
“Wakati CHADEMA tunataka spika na mawaziri wasitokane na
wabunge, CCM wao wamependekeza viongozi hao watokane na wabunge ili
waendelee kuwakandamiza Watanzania. CHADEMA tunataka nchi iwe na mawaziri
saba tu, na siyo 15 wa pendekezo la tume na 64 waliopo sasa.
“Si hilo tu, ibara ya 22 hadi 23 ya rasimu ya katiba
mpya, CCM kwa mapendekezo yao wanataka haki za binadamu zisiwepo kwenye
katiba mpya ijayo, bali ziwepo kwenye sheria tu. CCM haitaki kuwepo malengo
ya taifa kwenye katiba mpya!
“Tutakusanya saini milioni 10 za wananchi kuhusu
mapendekezo ya katiba mpya. Pia tutakusanya saini milioni tano za wananchi
kutaka tozo ya laini za simu ifutwe,” alisema Wenje huku akisisitiza
uundwaji wa serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Shirikisho.Mbunge wa
Biharamuro Magharibi, Dk. Mbasa, mbunge Conchesta, Katibu wa CHADEMA
Manispaa ya Bukoba, mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar pamoja
na mwenyekiti wa chama hicho Biharamulo Magharibi, Kasaiza waliishutumu
serikali kwa kushindwa kuwaondolea umasikini wananchi wake.
Walisema kwa sasa Watanzania walio wengi wanalazimika
kuvaa viatu vya ‘yebo yebo’ kwa sababu ya umasikini unaotokana na kushindwa
kwa Serikali ya CCM kuwatumikia wananchi wake kwa kuwanufaisha na
rasilimali zilizopo hapa nchini.
“Serikali ya chama tawala imekosa sifa ya kuwaongoza
wananchi. Tunahitaji tuungane wote kuiondoa CCM mwaka 2015. CHADEMA ni
mkombozi wa Watanzania na ndiyo maana wabunge na viongozi wake wanapambana
usiku na mchana kutwa kupigania maendeleo ya wananchi,” alisema Dk. Mb
asa
SOURCE TANZANIA DAIMA
|
0 comments:
Post a Comment