MAFANIKIO hutokana na jitihada katika maisha tunayoyaishi. Watu wengi wanaopenda kufanikiwa mara zote hutafuta mbinu mbalimbali ili kutimiza ndoto zao. Hivyo basi unatakiwa kuota ndoto ya mafanikio yenye malengo makubwa.
Binafsi ninaamini katika malengo hayo kuwa kuna mafanikio
endapo utamaanisha. Wakati mtu anapoanza kuwa na malengo makubwa, anaanza kwa
kufikiri jinsi Mungu alivyomwezesha katika jambo hata kufikia hatua na
kufanikiwa.
Ndoto hiyo ya mafanikio haina gharama, ni jinsi ya unavyoweza
kujipangia muda na ratiba zako. Kumbuka ukiwa na malengo ya mafanikio
haitakugharimu chochote.
Unaweza ukawa na malengo ya kuanzisha mradi mkubwa pasipokuwa
na fedha, inabakia kuwa ni ndoto tu. Mungu alianza kuumba dunia ikiwa haina
kitu. Tunaweza kuwa na malengo makubwa ya mafanikio katika maisha yetu,
haijalishi ni ya aina gani.
Unapokuwa na ndoto hiyo ya kutaka kufanikiwa, kamwe usiruhusu
moyo wako kuvunjika au kuwa katika hali ya kukata tamaa na wasiwasi. Kwani hali
hiyo itakudhoofisha na kukufanya usisonge mbele, bali urudi nyuma.
Unapohitaji jambo kubwa kutokea katika maisha yako unatakiwa
kuwa na maono mapya. Kumbuka hata wewe unaweza ukawa na maono makubwa ya ajabu.
Haijalishi ni mtu wa aina gani, umetoka wapi au umepatwa na
jambo gani, katika hali uliyonayo unaweza kuwa na maono mapya. Kumbuka malengo
makubwa hayawi kwa watu waliofanikiwa, bali ni kwa wale wanaotaka kufanikiwa.
Vyovyote uwazavyo, ndoto inainua na kuweka kitu kipya katika
maisha yetu, inatutengeneza na kutusogeza mbele, inatuwezesha kufikia malengo
makubwa tofauti na ilivyokuwa awali. Inatuwezesha kufanya kitu kikubwa ambacho
hatujawahi kukifanya tena kabla ya hapo.
Je, wataka kuwa fulani? Kusimama nje ya kusanyiko kubwa?
Kukumbukwa? Hali hiyo inakuwepo ndani ya mioyo yetu inayodunda na kutaka kupata
siri ya mafanikio.
Tunataka kuwa fulani. Inawezekana, ndiyo inawezekana. Mungu
ametoa kwa kila mtu uwezo na vipaji mbalimbali. Wakati Mungu anakuumba alikupa
kipaji na akasema kama utatumia kipaji ulichonacho atakiongeza, na kama
hutatumia kipaji ulichonacho utakipoteza. Kukitumia kipaji chako au kukiachia
ni juu yako wewe!
Dunia yetu imejaa vipaji vingi na uwezo ambao hautumiwi.
Unatakiwa kulima kwa bidii, na kupalilia ili upate mavuno bora. Tumia kipaji
chako kabla hujakipoteza.
Unaweza kudhani kuwa hauna kipaji chochote, si kweli, labda
inawezekana haujagundua kipaji chako. Inawezekana umekiweka kipaji chako kabatini.
Amini kuwa kila mmoja anacho kipaji chake alichopewa na Mungu.
Waweza kutumia kipaji ulichonacho au kukipoteza. Maisha yetu
yamejengwa katika kanuni hiyo. Kuna mifano mingi ya kupoteza au kupata, hiyo ni
kanuni ya kawaida.
Chukua hatua ambazo zitaifanya ndoto yako kuwa kweli. Ota
ndoto yenye thamani katika maisha yako. Kama hauna malengo, haitawezekana
matarajio yako kutimia. Ndoto inaanza unapokuwa na wazo. Kumbuka watu huvutiwa
na wenye maono makubwa.
Chagua maono yenye matarajio. Baadhi ya watu wanapoteza muda
wao kwa kuwa na malengo ambayo hayatawasaidia. Mfano, kuna kijana katika miaka
iliyopita alisaidiwa kupewa ushauri baada ya kupoteza muda wake mwingi
akifikiria ni jinsi gani ataweza kumpata mke wa jirani yake na kumfanya awe
wake. Ndoto yake hiyo haikuwa ya thamani ya muda mrefu.
Wakati wazo linapokujia katika ufahamu wako, iulize nafsi
yako maswali matatu. Je, jambo hilo litampendeza Mungu? Litawasaidia watu
wanaoteseka? Kwa maneno mengine litakuwa msaada kwa watu? Litaleta mafanikio
mazuri kwako? Kama jibu lako ni ndiyo katika maswali yote, utakuwa na maono
yenye mafanikio.
Unapoamua kufanya jambo fulani, usijiulize ulize kuwa hii ni
njia nyepesi ya mafanikio? Au ni njia rahisi? Inaweza kuwa na usalama?
Haitakuwa na vikwazo? Hakuna utakachoshindwa utakapofanya bidii. Hakuna mwenye
nguvu ya kuua ndoto yako, isipokuwa wewe mwenyewe.
Panga mipango vizuri kwa kuwa huwezi kujenga bila ramani.
Huwezi kufanikiwa matarajio yako pasipokuwa na malengo makubwa. Ninamfahamu mtu
aliyekuwa na maono makubwa lakini yalikuwa hayafiki mbali. Ni kwa sababu
alikuwa hana ramani ya maono yake.
Hakikisha unatimiza ndoto uliyojiwekea. Malengo yako hayawezi
kufanikiwa kama hujajitoa kufanya hivyo. Ili kufanikiwa katika mipango yako
unahitaji juhudi na kufanya kazi kwa bidii ili upate mafanikio.
Amua pa kuanzia. Fanya uamuzi sahihi. Panga muda wa kuanza.
Usitafute sababu ya kuacha kufanya malengo yako kwa muda ulioupanga. Katika
dunia yetu kuna watu wengi wenye mipango mingi lakini hawaifanikishi. Jiondoe
katika kundi hilo. Fanya kitu. Andika barua, piga simu. Anza hatua ya
mafanikio.
Jiamini waweza kutimiza ndoto zako. Wakati unajaribu kupata
mafanikio utaona kuwa ni kipindi kigumu kwako. Hali ya kukata tamaa inakuwepo
katika moyo wako, ikisema jiondoe katika hatua ambayo unataka kuianza ya kupata
mafanikio katika maisha yako, kataa.
Kama unakutana na kipindi cha majaribio katika biashara,
ndoa, mambo yako binafsi, kwenye wingi wa watu au hali ya maisha uliyoizoea na
uko tayari kukabiliana nayo, songa mbele usikate tamaa.
Unachofanya ni kujaribu kupata mafanikio, tena mafanikio
makubwa. Katika kila mafanikio unayoyapata, kuna gharama ya kulipa. Kumbuka
huwezi kupata ushindi bila kulipa gharama.
CREDIT:LUCY NGOWI
Karibu tena kuitembelea blog hii
wako faraja mmasa
************Tafuta maisha mazuri na kufanikiwa kama utaishi milele lakini kumbuka kumcha mungu kama leo ndio siku yako ya mwisho kuwa duniani***********
0 comments:
Post a Comment