Moja ya nguzo za mafanikio ya wajasiriamali ni
elimu, ikwemo ya kuwaongezea upeo wa kutafuta mitaji.
Ni ijumaa nyingine tunapokutana tena katika
kona hii ya mjasiriamali, hii ni kona ambayo maudhui yake ni kuona namna bora
ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kuanzisha na baadae kuendeleza
biashara zao na kupata mafanikio wanayotamani.
Makala iliyopita ilijadili juu ya umuhimu wa
kuweka akiba ili kujikinga na majanga.
Kuna msemo unasema akiba haiozi, mjasirimali
unapaswa wakati wote kukumbuka msemo huu ili uwe chachu ya wewe kujiwekea akiba
kwa malengo mbalimbali.
Ukiwa na utamaduni wa kujiwekea akiba kutokana
na mapato yako unayoyapata utakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kukabilina na
majanga mbalimbali ambayo yanaweza kutokea katika biashara yako, kumbuka una
nafasi ya kubadilika na kujipanga upya.
Leo katika kona ya mjasiriamali tutakumbushana
juu ya baadhi ya njia ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kuweza
kuongeza mitaji ya biashara zao. Katika njia mbalimbali za kuongeza mitaji zipo
zinazoweza kusaidia na nyingine kuumiza.
Mitaji ya biashara ni kilio cha wengi aidha
kwa wale walio katika ujasiriamali au kwa wale wenye nia ya kuingia kwenye
ujasiriamali. Wengi hulia kwamba watapata wapi mtaji kwaajili ya kuanzisha
biashara au kwaajili ya kuendeleza biashara.
Wajasiriamali wanapaswa waelewe kwamba kuna
njia mbalimbali za kuweza kuongeza mtaji katika biashara wanazofanya. Muhimu
zaidi ni kufahamu njia hizi ili kuweza kuangali ni ipi kwa hatua uliyofikia
inaweza kukusaidia zaidi badala ya kukuumiza.
Yafaa pia kujiuliza je ni sababu zipi
zinazopelekea wewe kuwa na hitaji la ongezeko la mtaji katika biashara
yako na nini matokeo tarajiwa. Kujiuliza
maswali haya na mengine itakusaidi kufanya uamuzi sahii. Zifuatazo ni njia za
kuongeza mitaji ya biashara yako.
Njia ya kwanza ni uwekaji wa akiba. Uwekaji wa
akiba ni njia ya kwanza ambayo inaweza kukusaidia katika kukuza mtaji wako wa
biashara. Kma utakuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ni rahisi kwako kutumia
akiba ili uweze kukuza mtaji wako.
Iwe kwa mjasiriamali mwenye biashara mpya au
inayoendelea ni muhimu sana kufikiria kutumia njia hii ili kuweza kukuza mtaji
wa biashara. Uwekaji wa akiba ni moja ya njia ya kukuza mtaji ambayo haina gharama wala matatizo
kuliko nyingine yoyote.
Uwekaji wa akiba ni njia inayoonekana ngumu
kati ya watu kwasababu ni njia ambayo inahitaji nidhamu ya hali ya juu.
Unapotaka kutumia njia hii ili kuweza kukuza mtaji wa biashara au kuendeleza
biashara unahitaji nidhamu katika matumizi ya fedha zako.
Jiulize je matumizi ya fedha zako yakoje? Ni
yapi yamekuwa matumizi ya msingi na yapi si ya msingi, kwanini usipunguze au
kuacha matumizi yasio ya msingi na kuweka akiba ili kuweza kukuza mtaji
kwaajili ya biashara yako.
Jiulize unatumia kiasi gani cha fedha zako
kwaajili ya ‘vocha’, unatumia kiasi gani kwaajili ya pombe, unatumia kiasi gani
kwaajili ya starehe, vipi michango ya harusi, je unatumia kiasi gani kwaajili
ya burudani nyingine ambazo si za msingi!
Kaa chini na utafakari juu ya mapato na
matumizi yako na angalia ni kwa namna gani unaweza kuweka sehemu ya mapato yako
kama akiba kwaajili ya aidha kukuza mtaji wa biashara unayofanya au kuanzisha
biashara mpya na malengo mengine ya baadae.
Njia ya pili ni kupitia ndugu wa familia au
mrafiki. Wapo wajasiriamali ambao wamefanikiwa kupitia ndugu au marafiki. Kuna
msemo unasema hupaswi kumpa mtu samaki bali umfundishe jinsi ya kuvua samaki.
Ndugu wa familia au marafiki ni watu ambao
wanaweza kukusaidia kuweza kukuza mtaji kwaajili ya kuanzisha au kuendeleza
biashara. Yafaa kutafuta namna bora ya kuweza kukaa na ndugu au rafiki ili
kuweza kumshawishi ni kwa namna gani akusaidie.
Ni muhimu kwa mjasiriamali kutoa pendekezo
lenye kufaa kwa ndugu au rafiki mwenye uwezo ili kuweza kumshawishi juu ya
uwekezaji katika jambo fulani ambalo lina matokeo fulani tarajiwa na
vihatarishi vyake na namna ya kuviepuka.
Katika msemo wa usimpe mtu samaki bali
mfundishe namna ya kuvua samaki. Maana yake ni kwamba angalia namna unavoweza
kumsaidia mtu aweze kujisaidia mwenyewe hasa katika ujasiriamali, si lazima
umpatie fedha bali unaweza kumpa vifaa au nyenzo.
Kutumia njia hii ya ndugu au marafiki katika
kukuza mtaji wa biashara wakati mwingine kunaweza kuleta matatizo miongoni mwa
wana ndugu au marafiki, hivyo katika matumizi ya njia mambo yote yafaa yawekwe
wazi ili kuepuka matatizo.
Njia ya tatu ya kuweza kukuza mtaji wa
biashara ni kuingia ubia (partnership). Kuingia ubia ni njia inayowakutaniasha
watu ambao mahitaji yao yanafana ila upande mmoja unaweza ukawa una hili na
mwingine umekosa hili hivyo inabidi kuungana.
Kwa mafano kama wewe una mali X na umekosa
mali Y ili kuweza kufanya jambo fulani basi unaweza kuingia ubia na mtu mwenye
mali Y ili kila mmoja aweze kufikia malengo yake husika. Makampuni yanaingia
ubia itakuwaje kwa nyinyi wajasiriamali!
Pamoja na njia ya ubia kama namna ya kukuza
mtaji wa biashara, jambo hili limekuwa gumu kwa watu wengi kwani badala ya
kutumia njia hii kujijengea maendeleo wabia wengi wamejikuta wameingia kwenye
‘bifu’ zisizo na msingi na hatimaye kushindwa.
Njia ya nne ya kuweza kukuza mtaji wa biashara
ni kutumia mikopo. Hii ni njia kubwa zaidi inayotumiwa na wajasiriamali katika
kukuza mitaji ya biashara zao. Ni njia ambayo inahusisha gharama na ambayo
imewaacha baadhi ya wajasiriamali katika matatizo.
Wajasiriamali wengi wamekuwa wakitumia Benki,
SACCOS, VICOBA na taasisi nyingine za mikopo midogo (Microfinance Institutions)
kutafuta fedha ili kuweza kukuza mitaji ya biashara zao. Nashauri, mikopo si ya
kukimbilia yafaa kujiuliza kwanza.
Kuepuka matatizo ya kukuza mtaji kwa njia ya
mikopo toka taasisi mbalimbali za fedha, yafaa mjasiriamali kujiuliza baadhi ya
maswali, lengo kuu la kujiuliza maswali haya ni kuweza kujifanyia tathmini kama
kweli unahitaji kukuza mtaji kwa njia ya mkopo.
Swali la kwanza jiulize, je una malengo gani
na fedha utakazokopa? Je malengo uliyonayo juu ya mkopo unaoomba yana
vihatarishi vipi, hii ni kwasababu taasisi nyingi za fedha hupenda kutoa mikopo
kwenye shughuli ambazo zina usalama na endelevu.
Swali la pili la kujiuliza, je unahitaji kiasi
gani cha fedha ili kuweza kukuza mtaji wa biashara yako ? Kuna wajasiriamali
ambao huenda kukopa lakini hawajui wanahitaji kiasi gani, hawajajipanga !
Wanachojua wanataka kukopa tu, mambo mengine baadae.
Swali la tatu la kujiuliza, ni lini hasa
unahitaji mkopo huo ? Wapo ambao wanakopa kwanza halafu baada ya kupata mkopo
ndio wanakaa chini kupanga mipango. Kaa chini ujiulize kama kweli unataka mkopo
ungependa upate lini huo mkopo na kwanini.
Swali la nne la kujiuliza ni, je utahitaji
mkopo huo kwa muda gani ? Kama utahitaji mkopo kwa muda mfupi na kwasababu
zinazoeleweka, itakuwa rahisi kwako kushawishi taasisi ya fedha kukupatia mkopo
badala ya kukaa bila kujua muda wa hitaji lako.
Swali la tano na la msingi ni juu ulipwaji wa
mkopo, ukiomba mkopo na kupewa je utaulipaje ? Je una vyanzo gani vya mapato
ambavyo unaweza kuvitumia katika kuhakikisha mkopo unarejeshwa pamoja na
gharama zake (riba) kwa muda uliopangwa .
Swali la sita la kujiuliza ni ikiwa mambo
yataenda mlama, nini kitafanya mkopo ubaki
salama ? Hapa wakopeshaji wengi huhitaji dhamana za mkopo (collateral)
ili kuweza kwa namna moja au nyingine kuulinda mkopo uliotolewa ili ubaki
salama, kulipika!
Ni matumaini yangu ndugu mjasiriamali, katika
kutafuta namana bora ya kukuza mtaji wa biashara yako utaangalia ile ambayo
inaendana na hali halisi uliyonayo badala ya kukurupuka au kufuata mkumbo, kwa
njia hii utaweza kuepuka matatizo yasiyo lazima
.
KAMA UNAHITAJI USHAURI WOWOTE KUHUSU BIASHARA UNAWEZA PIGA NAMBA 0658494977
SOURCE: KONA YA MJASIRIAMALI (NIPASHE).
WAKO FARAJA MMASA
+X3p
0 comments:
Post a Comment